Monday 4 September 2017

FARAJA YAPATA UGENI KUTOKA PAROKIA YA SORGENFRI DENMARK

Shirika la Faraja Trust Fund lilipata ugeni kutoka parokia ya Sorgenfri nchini Denmark ambao ni wahisani mradi wa kuwasaidia watoto yatima na watoto wa mtaani kupata haki ya msingi ya elimu mradi unaojulikana kama Street Side Schools (SSS) unaoendeshwa na shirika tangu mwaka 1997.
Ugeni huo uliowakilishwa na wachungaji wawili ambao ni Mchungaji Frances Benzon na Mchungaji Anne Katrine Sylvest wakiwa na mwenyeji wao Mchungaji Pindua ambaye ni msaidizi wa askofu kanisa la KKKT Morogoro.
Kutoka kulia ni Mchungaji Frances Benzon (Sorgenfri Denmark), Mchungaji Anne Katrine Sylvest (Sorgenfri Denmark), Dr Lucy Nkya (Mkurugenzi Faraja Trust Fund), Mchungaji Pindua (Msaidizi wa askofu KKKT Morogoro), Ndugu Lazaro Meshack (Afisa Utawala Faraja Trust fund).
Mkurugenzi wa Faraja Trust Fund Dr Lucy Nkya aliwakaribisha wageni na kuanza maongezi ambapo alianza kwa kutoa historia fupi ya shirika ya toka lianzishwe mwaka 1991 hadi sasa na nini limefanya na linaendelea kufanya kwa jamii.
Mkurugenzi Dr. Lucy Nkya aliwaeleza wageni hao kutoka Denmark kua mradi wa SSS unawasaidi watoto yatima na wa mtaani ambao umri wao umepita miaka 7 kupata haki ya elimu hadi darasa la nne ambapo wanafanya mtihani pamoja na wanafunzi walio kwenye mfumo rasmi wa serikali na wanapofaulu wanaingia kwenye mfumo rasmi wa shule za msingi kwani kwa mfumo rasmi unachukua wanafunzi wasiozidi miaka 7 na akaongezea wengi wa wanafunzi wanaosoma katika shule za faraja ni wale wenye umri kuanzia miaka 10 hadi 15. Watoto wote wanaosoma kwenye shule za shirika ni yatima ambao wengi wamepoteza wazazi wao kutokana na maradhi mbalimbali ukiwemo VVU. Vituo vipo viwili ambapo kimoja kipo mtaa wa Mwere na kingine Chamwino. Vituo hivi vina msaada mkubwa sana kwa watoto yatima kwani ndiovituo pekee katika manispaa ya Morogoro kwa ajili ya kuwasaidia watoto yatima hivyo alitoa shukrani kwa wahisani hao kutoka Denmark kwa kufanikisha watoto yatima kupata haki ya elimu.
Mkurugenzi aliwaeleza kwamba watoto wote wanasomeshwa bure pamoja na kupewa mahitaji mengine ya shule ikiwemo sare za shule, madaftari pamoja na huduma ya chakula hasa kunywa uji. Pia mkurugenzi aligusia changamoto kubwa inayoikabili shirika katika uendeshaji wa shule hizo ni kukosekana kwa kiasi cha fedha cha kutosha kinachohitajika kuwalipa wanafunzi, kulipia huduma za maji na umeme pamoja na gharama inayoambatana na huduma ya kuwapa uji.
Ukiachilia mbali mradi wa SSS, Mkurugenzi aliwagusia kuhusu miradi mingine ambayo inatarajiwa kuanzishwa na shirika endapo itapata nguvu ya fedha kutoka kwa wahisani, miradi hiyo ni Young Mothers Project kwa ajili ya kuwasaidia watoto wanaoachishwa shule kutokana na kupata mimba ambapo shirika litawasaidia kuwapa mafunzo ya ufundi ili iwasaidie kuendesha maisha yao na watoto watakaozaa ili kuepusha matatizo ya watoto wa mitaani. Mradi mwengine ni kwa ajili ya kupunguza tatizo la ajira kwa vijana ambao unajulikana kama Ujana ni Mtaji Program.
Mchungaji Frances pamoja na mchungaji Anne walifurahishwa sana na jitihada za shirika katika kusaidia jamii hivyo waliahidi kufikisha changamoto zilizoainishwa na mkurugenzi kwa Uongozi wa kanisa lao watakaporudi Denmark ili waone ni kwa namna gani wanaweza kusaidia nia nzuri ya shirika katika kuwasaidia watu wa makundi mbalimbali ambao wanauhitaji.
Baada ya mazungumzo mengi, Mkurugenzi Dr. Lucy Nkya aliwatembeza wageni kuona vitengo mbalimbali vinavyopatikana katika ofisi ya shirika.
Kitengo cha msaada wa kisheria
Katika ofisi kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria ambapo wananchi wengi wasio na uwezo wa kulipia gharama kubwa kwa wanasheria huwa wanakuja na kuhudumiwa bila malipo. Mkuu wa kitengo cha sheria Ndugu Derick Vincent alisema wengi wanaokuja wanahitaji msaada wa kisheria upande wa ardhi pamoja na matatizo ya mirathi.

Mkurugenzi na wageni wakiwa katika ofisi ya kitengo cha IT
Ofisi ya kitengo cha mafunzo
Vitengo vingine ambavyo mkurugenzi aliwatembeza wageni ni pamoja na ofisi ya mhasibu, ofisi ya afisa utawala, ofisi ya lishe, ofisi ya ujana ni mtaji programu na ofisi ya USAID Boresha Afya.

Baada ya zoezi la utambezi kwa vitengo vinavyopatikana ofisi ya Faraja Trust Fund, Wageni walipata fursa ya kwenda kutembelea shule kwa ajili ya mradi wa SSS iliyopo mtaa mwere, kata ya Kingo.
Mkurugenzi Dr Lucy Nkya akiwaeleza jambo wageni walipofika maeneo ya mwere ilipo shule.





Katika kituo cha mwere, mkurugenzi aliwatambulisha wageni kwa uongozi wa kituo pamoja na wanafunzi ambapo baada ya hapo walipewa maelezo mafupi kuhusu kituo zikiwemo changamoto mbalimbali. Kwa bahati nzuri wageni waliwakuta wanafunzi wakipata uji hivyo walishuhudia jinsi shirika la Faraja Trust Fund linavyojishughulisha na kufanya matumizi vizuri kwa kile kidogo wanachopata kutoka kwa wahisani wao.
Mkurugenzi Dr Lucy Nkya aliwapa nafasi ya wageni kuongea na watoto ambapo walijitambulisha pia walitoa salamu za kutoka parokia yao nchini Denmark na baadae walitoa zawadi kwa watoto ambayo ilikabidhiwa kwa watoto kupitia viongozi wao.

Kwa niaba ya wanafuzi wengine, kaka mkuu alishukuru sana kwa msaada na zawadi wanazopata kutoka kwa wahisani hao ambao unafanya mradi uwe enderevu. 
Kabla ya safari ya kwenda Chamwino kwenye kituo kilicho chini ya mradi wa SSS, mkurugenzi, wafanyakazi na wanafunzi walipiga picha moja na wageni kwa ajili ya kumbukumbu za mradi na shirika kiujumla.
Baada ya wageni kuagwa na uongozi wa kituo na wanafunzi, msafara wa kwenda kwenye kituo cha Chamwino ulianza.


Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Dr Lucy Nkya, Mchungaji Frances Benzon na  Mchungaji Anne Katrine Sylvest wakiwa katika kituo cha Chamwino 
wanafunzi wa kituo cha Chamwino


Baada ya utambulisho, ulikua ni mda wa kupata uji ambapo sio watoto tu bali hadi wageni nao walipewa uji ili wanywe na wajionee wenyewe watoto wanachopatiwa watoto kutokana na msaada wao wanaotoa kupitia shirika la Faraja Trust Fund.

Mwakilishi wa kituo cha chamwino upande wa wanafunzi ambaye ndiye kaka mkuu, alishukuru sana wageni hao na kuwaomba waendelee kutoa msaada kwa kituo ili kiweze kufikia malengo na akaelezea changamoto zikiwemo uboreshwaji wa vyoo, kujengwa ukuta na mahitaji mengine yakila siku ambayo ni muhimu kwa uendeshaji wa kituo.
Kwa niaba ya parokia ya Sorgenfri, mchungaji Frances alifurahi kwa mapokezi na akaahidi kufikisha chanagamoto hizo watakaporudi Denmark. Baada ya hapo, akakabidhi zawadi kwa kiongozi wa wanafunzi.
Baada ya kukabidhiwa zawadi, watoto walifurahi na waliwaimbia wimbo wa shule kabla ya wageni kuondoka kuendelea na ratiba nyengine.
Picha ya pamoja ya wageni ,uongozi wa kituo na shirika la Faraja Trust Fund

Kwa nafasi ya pekee, wageni walipata fursa ya kuoneshwa maeneo ya kituo na kujionea baadhi ya changamoto zinazozikabili kituo hasa upande wa miundominu.

Kwa niaba ya shirika la Faraja Trust Fund, Mkurugenzi Dr Lucy Nkya alitoa shukrani zake za dhati na akawahakikishia ushirikiano katika kutekeleza miradi ya kusaidia jamii hasa jamii yenye uhitaji na hata wanapotoa ufadhili wawe na uhakika na shirika katika utekelezaji.

SHARE THIS

Author:

Facebook Comment

0 comments: