Friday 18 August 2017

MAZISHI YA MAREHEMU MZEE DICKSON SANGALI

Shirika la Faraja Trust Fund lilipata msiba mzito wa aliyekua dereva wa shirika kwa kipindi kirefu mzee Dickson Sangali, aliyefariki jumatatu ya tarehe 14 mwezi Agosti, 2017.
Wakati wa mazishi ya mzee wetu mpendwa Dickson Sangali 

Msiba ulikua nyumbani kwa marehemu maeneo ya Mazimbu, Morogoro mjini. Shirika la Faraja Trust Fund lilishiriki kikamilifu katika safari ya mwisho ya mzee wetu Dickson Sangali ambapo toka akiwa mgonjwa hadi umauti unamfika, Shirika lilisaidiana na familia ya marehemu.

Mazishi ya mzee wetu Dickson Sangali yalifanyika siku ya jumatano tarehe 16 mwezi wa agosti, 2017 ambapo yalianza na ibada nyumbani kwa marehemu. Baada ya ibada kulifatiwa na salamu za rambirambi kutoka sehemu mbalimbali kama vile kutoka kwa mwakilishi wa kata (Diwani wa kata ya Mazimbu), Mkurugenzi wa Faraja Trust Fund bila kusahau neno la shukrani kutoka kwa mwakilishi wa familia ya marehemu Dickson Sangali.

Kwa niaba ya shirika la Faraja Trust Fund mkurugenzi Dr. Lucy Nkya alizungumza machache juu ya marehemu mzee Dickson Sangali. Mkurugenzi alisema "Dickson alikua dereva lakini pia alikua ni mlezi na msaidizi wa wagonjwa na wazee waliokua wanahitaji huduma na msaada kutoka Faraja". Mkurugenzi Dr. Lucy Nkya alisisitiza kwa kutoa mfano "Kuna marehemu mama Hadija Sued, Dickson alijitolea kua mtoto wake kwasababu alikua hana mtoto, akiumwa  akipiga simu Dickson alikua anakwenda anamkogesha anambeba anampeleka hospitali. Akikutwa hajanywa uji, Dickson huyu huyu anapika uji anamlisha".
Mkurugenzi wa Faraja Trust Fund, Dr.Lucy Nkya alikua anatoa salamu za rambirambi kwa niaba ya shirika.
Pia mkurugenzi aligusia maisha ya marehemu mzee Dickson na jamii nyingine ikiwemo familia na shirika la Faraja Trust Fund akisema "Kila mmoja alikua anamuita Uncle Dick kwasababu alikua anaupendo, alikua na upole kwake kulikua hakuna kijana, hakuna mzee, hakuna masikini wala tajiri".
Mkurugenzi akimuelezea marehemu mzee Dickson Sangali kwa majonzi na hisia kubwa.
Mkurugenzi hakusahau kuwasihi watu ambao walihudhuria msiba wa mzee Dickson Sangali kufuata yote mazuri ambapo alisema "Kwanza ni uvumilivu, kumsikiliza mtu hata kama mtu anakunyooshea kidole kwa jambo ambalo hukulifanya, msikilize kwanza ndo uweze kujitetea sio kuanza kubishana nae".  Aliendelea kusisitiza "Ndugu zangu, alitekeleza ile amri kuu ya mapendo lakini kubwa zaidi ni UADIRIFU".

Baada ya salamu za rambirambi kutoka kwa makundi tofauti, safari ya kuelekea Magubike kwa ajili ya mazishi ilianza.
Jeneza lililobeba mwili wa marehemu Mzee Dickson Sangali likipakizwa ndani ya gari tayari kwa safari ya kuelekea Magubike kwa ajili ya mazishi.

Msafara ulifika salama kijiji cha Magubike ambapo shughuli ya mazishi ilitakiwa kufanyika. Mwili wa marehemu ulipelekwa nyumbani na baada ya hapo kanisani kwa ajili ya ibada na mwisho kupumzisha katika makaburi ya familia.





Baada ya shughuli ya kuaga mwili wa marehemu Mzee Dickson Sangali, msafara uliekea kanisani kwa ajili ya ibada.

Ikafika mda wa kuelekea makaburini na kupumzisha mpendwa wetu, mzee wetu Dickson Sangali.




Mke wa marehemu akiweka mashada kwenye kaburi la marehemu mme wake mzee Dickson Sangali


Kaburi la mpendwa mzee wetu Dickson Sangali
Mara baada ya mazishi, safari ya kurudi morogoro mjini nyumbani kwa marehemu Dickson Sangali ilianza.


Kwa niaba ya familia, mtoto mkubwa wa kiume wa marehemu mzee Dickson Sangali, Michael Sangali alitoa shukrani zake za dhati kwa shirika kwa ushirikiano ulioneshwa wakati wote kuanzia ugojwa hadi kifo cha marehemu baba yao.

Mkurugenzi wa Faraja Trust Fund Dr. Lucy Nkya aliahidi familia yake pamoja na shirika itatafuta siku rasmi kwa ajili ya kuwatembelea na kuwapa pole.
Marehemu mzee Dickson Sangali alikua anasumbuliwa na malazi ya moyo na mapafu ambapo alilazwa kwa vipindi tofauti katika hospitali ya mkoa wa Morogoro kabla ya kuhamishiwa hospitali ya taifa Muhimbili ambapo mauti yalimkuta tarehe 14 agosti, 2017.
Marehemu ameacha mke mmoja, watoto nane, wajukuu ishirini na nne na vitukuu vinne.

"BWANA AMETOA NA BWANA AMETWAA, JINA LAKE LIHIMIDIWE"


SHARE THIS

Author:

Facebook Comment

0 comments: