Friday 18 August 2017

MAZISHI YA MAREHEMU MZEE DICKSON SANGALI

MAZISHI YA MAREHEMU MZEE DICKSON SANGALI

Shirika la Faraja Trust Fund lilipata msiba mzito wa aliyekua dereva wa shirika kwa kipindi kirefu mzee Dickson Sangali, aliyefariki jumatatu ya tarehe 14 mwezi Agosti, 2017.
Wakati wa mazishi ya mzee wetu mpendwa Dickson Sangali 

Msiba ulikua nyumbani kwa marehemu maeneo ya Mazimbu, Morogoro mjini. Shirika la Faraja Trust Fund lilishiriki kikamilifu katika safari ya mwisho ya mzee wetu Dickson Sangali ambapo toka akiwa mgonjwa hadi umauti unamfika, Shirika lilisaidiana na familia ya marehemu.

Mazishi ya mzee wetu Dickson Sangali yalifanyika siku ya jumatano tarehe 16 mwezi wa agosti, 2017 ambapo yalianza na ibada nyumbani kwa marehemu. Baada ya ibada kulifatiwa na salamu za rambirambi kutoka sehemu mbalimbali kama vile kutoka kwa mwakilishi wa kata (Diwani wa kata ya Mazimbu), Mkurugenzi wa Faraja Trust Fund bila kusahau neno la shukrani kutoka kwa mwakilishi wa familia ya marehemu Dickson Sangali.

Kwa niaba ya shirika la Faraja Trust Fund mkurugenzi Dr. Lucy Nkya alizungumza machache juu ya marehemu mzee Dickson Sangali. Mkurugenzi alisema "Dickson alikua dereva lakini pia alikua ni mlezi na msaidizi wa wagonjwa na wazee waliokua wanahitaji huduma na msaada kutoka Faraja". Mkurugenzi Dr. Lucy Nkya alisisitiza kwa kutoa mfano "Kuna marehemu mama Hadija Sued, Dickson alijitolea kua mtoto wake kwasababu alikua hana mtoto, akiumwa  akipiga simu Dickson alikua anakwenda anamkogesha anambeba anampeleka hospitali. Akikutwa hajanywa uji, Dickson huyu huyu anapika uji anamlisha".
Mkurugenzi wa Faraja Trust Fund, Dr.Lucy Nkya alikua anatoa salamu za rambirambi kwa niaba ya shirika.
Pia mkurugenzi aligusia maisha ya marehemu mzee Dickson na jamii nyingine ikiwemo familia na shirika la Faraja Trust Fund akisema "Kila mmoja alikua anamuita Uncle Dick kwasababu alikua anaupendo, alikua na upole kwake kulikua hakuna kijana, hakuna mzee, hakuna masikini wala tajiri".
Mkurugenzi akimuelezea marehemu mzee Dickson Sangali kwa majonzi na hisia kubwa.
Mkurugenzi hakusahau kuwasihi watu ambao walihudhuria msiba wa mzee Dickson Sangali kufuata yote mazuri ambapo alisema "Kwanza ni uvumilivu, kumsikiliza mtu hata kama mtu anakunyooshea kidole kwa jambo ambalo hukulifanya, msikilize kwanza ndo uweze kujitetea sio kuanza kubishana nae".  Aliendelea kusisitiza "Ndugu zangu, alitekeleza ile amri kuu ya mapendo lakini kubwa zaidi ni UADIRIFU".

Baada ya salamu za rambirambi kutoka kwa makundi tofauti, safari ya kuelekea Magubike kwa ajili ya mazishi ilianza.
Jeneza lililobeba mwili wa marehemu Mzee Dickson Sangali likipakizwa ndani ya gari tayari kwa safari ya kuelekea Magubike kwa ajili ya mazishi.

Msafara ulifika salama kijiji cha Magubike ambapo shughuli ya mazishi ilitakiwa kufanyika. Mwili wa marehemu ulipelekwa nyumbani na baada ya hapo kanisani kwa ajili ya ibada na mwisho kupumzisha katika makaburi ya familia.





Baada ya shughuli ya kuaga mwili wa marehemu Mzee Dickson Sangali, msafara uliekea kanisani kwa ajili ya ibada.

Ikafika mda wa kuelekea makaburini na kupumzisha mpendwa wetu, mzee wetu Dickson Sangali.




Mke wa marehemu akiweka mashada kwenye kaburi la marehemu mme wake mzee Dickson Sangali


Kaburi la mpendwa mzee wetu Dickson Sangali
Mara baada ya mazishi, safari ya kurudi morogoro mjini nyumbani kwa marehemu Dickson Sangali ilianza.


Kwa niaba ya familia, mtoto mkubwa wa kiume wa marehemu mzee Dickson Sangali, Michael Sangali alitoa shukrani zake za dhati kwa shirika kwa ushirikiano ulioneshwa wakati wote kuanzia ugojwa hadi kifo cha marehemu baba yao.

Mkurugenzi wa Faraja Trust Fund Dr. Lucy Nkya aliahidi familia yake pamoja na shirika itatafuta siku rasmi kwa ajili ya kuwatembelea na kuwapa pole.
Marehemu mzee Dickson Sangali alikua anasumbuliwa na malazi ya moyo na mapafu ambapo alilazwa kwa vipindi tofauti katika hospitali ya mkoa wa Morogoro kabla ya kuhamishiwa hospitali ya taifa Muhimbili ambapo mauti yalimkuta tarehe 14 agosti, 2017.
Marehemu ameacha mke mmoja, watoto nane, wajukuu ishirini na nne na vitukuu vinne.

"BWANA AMETOA NA BWANA AMETWAA, JINA LAKE LIHIMIDIWE"

Saturday 12 August 2017

USHIRIKI WA UJANA NI MTAJI PROGRAM KATIKA MAONESHO YA 25 NANENANE MOROGORO

USHIRIKI WA UJANA NI MTAJI PROGRAM KATIKA MAONESHO YA 25 NANENANE MOROGORO

Mchoraji akiwa kazini akiandika kilichokua kinatarajiwa kufannywa na timu ya Ujana ni Mtaji.
Timu ya Ujana ni Mtaji iliyochini ya taasisi ya Faraja Trust Fund ikishirikiana na taasisi ya vijana inayojulikana kama Lights Up Youth Foundation ilishiriki maonesho ya 25 ya nanenane yaliyofanyika katika viwanja vya Mwl. Nyerere Morogoro yaliyokua na kauli mbiu  ZALISHA KWA TIJA MAZAO NA BIDHAA ZA KILIMO ,MFUGO NA UVUVI ILI KUFIKA UCHUMI WA KATI".kuanzia agosti 1-10.

Katika maonesho hayo Ujana ni Mtaji ilifanya baadhi ya shughuli ambazo ni Kutoa elimu ya lishe, Kupima uwiano wa mwili (BMI), Msaada wa kisheria, Elimu ya ujasiriamali pamoja na kutoa ushauri nasaha na kupima virusi vya ukimwi (VVU) kwa hiari. Ushiriki huu wa Ujana ni Mtaji ni kwa mara ya kwanza lengo likiwa kuwafikia watanzania wengi zaidi hasa wenye uhitaji wakiwemo wakulima.
Wanafunzi kutoka shule ya wasichana Ifakara wakipata maelezo mbalimbali kutoka kwa timu ya Ujana ni Mtaji.
Tulitembelewa na watu kutoka makundi tofauti kutoka katika jamii zetu wakiwemo watoto, wafugaji, wakulima wa kawaida, watu wa makundi maalumu, viongozi wa dini na viongozi wa serikali. Idadi ya waliotembelea banda letu ilikua kubwa na tunashukuru kwa wote waliojitokeza na kupata huduma kutoka kwa timu ya Ujana ni Mtaji.
Mtoto akipimwa uzito wakati wa maonesho ya 25 nanenane viwanja vya Mwl Nyerere, Morogoro.
Mfugaji jamii ya masai akipewa ushauri kuhusiana na masuala ya lishe baada ya kupima uwiano wa mwili 



Wachekeshaji walipita pia katika banda la Ujana ni Mtaji kupata elimu






Pia katika maonesho hayo banda la Ujana ni Mtaji lilitembelewa na Meya wa Manispaa ya Morogoro mjini Mh. Pascal Kihanga ambaye alielezwa kuhusiana na program kwa ufupi na alishiriki katika vipimo vya uwiano wa mwili pamoja na kupata elimu ya lishe bila kusahau alimalizia sehemu iliyohusu elimu ya ujasiriamali na msaada wa kisheria.
Mh. Pascal Kihanga ambaye ni Meya wa manispaa ya Morogoro akielezwa kwa ufupi kuhusiana na programu





Ndugu Yahya Naniya (kulia) kutoka ofisi ya mkuu wa wilaya Morogoro ambaye ndiye alikua mwenyeji wa Meya akisikiliza jambo kwa makini.
Ujana ni Mtaji inaamini kwenye nguvu na mchango wa wanawake katika maendeleo hasa kuelekea uchumi wa kati na kwa bahati njema tulitembelewa na mke wa mkuu wa mkoa wa Morogoro Mama Leonia Kebwe ambapo alihudumiwa vizuri na timu ya vijana ya Ujana ni Mtaji programu na furaha aliyoondoka nayo kwetu ni baraka tosha.


Kwa njia ya pekee tunatambua mwitikio na shauku ya wananchi katika kujua afya zao, sio upande wa uwiano wa mwili bali hadi kwenye kupima maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) bila kusahau ushauri nasaha.
Sehemu mahsusi iliyokua inatumika kwa ajili ya ushauri nasaha pamoja na kupima virusi vya ukimwi (VVU) kwa hiari



Pia Uongozi wa taasisi shiriki unatoa shukrani za dhati kwa wote waliojitokeza kwa njia moja au nyengine kuwakaribisha watu katika banda letu la Ujana ni Mtaji wakati wote wa maonesho.

Ujana ni Mtaji programu bado ipo kwenye mchakato wa ufunguzi ambao unatarajiwa kufanyika mda sio mrefu ambapo unaratibiwa na kamati maalumu inayoundwa kwa kushirikiana kwa taasisi za FARAJA TRUST FUND na LIGHTS UP YOUTH FOUNDATION pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa kushirikiana na ofisi ya mkurugenzi, mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa Morogoro.
Kamati ya maandalizi ya programu ya Ujana ni Mtaji iliyokutana tarehe 25 mwezi wa tano mwaka huu katika ofisi za Faraja Trust Fund.